Kenya na Marekani zimesaini mwafaka wa ushirikiano unaolenga kuimarisha utendakazi wa majeshi ya mataifa hayo mawili.
Waziri wa Ulinzi Aden Duale na mwenzake wa Marekani Lloyd Austin, wamesaini mkataba huo Jumatatu katika makao makuu ya jeshi la Kenya.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa baina ya mwaka 2023 hadi mwaka 2028 na yatasaidia nchi hizo mbili kuimarisha ushirikiano wa ulinzi kupitia teknolojia, uvumbuzi, kukabiliana na ugaidi, mafunzo ya pamoja na usalama wa usafiri wa majini ambao utawezesha majeshi ya nchi zote mbili kuwa tayari kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Austin aliunga mkono hatua ya Kenya kutuma majeshi kusaidia kulinda usalama nchini Haiti akiongeza kuwa Marekani itatoa msaada wa fedha ili kufanikisha mpango huo.