Kenya na Hungary zimepangiwa kutia saini Mikataba ya Maelewano katika nyanja za elimu na kilimo.
Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi atatia saini mikataba hiyo kwa niaba ya Kenya.
Mudavadi aliondoka nchini leo Jumatatu kuelekea Budapest kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary Péter Szijjártó aliyezuru Kenya mapema mwaka jana.
“Mkuu wa Mawaziri kwa niaba ya Kenya atatia saini Mikataba miwili ya Maelewano kati ya Kenya na Hungary katika nyanja za: Elimu na Kilimo,” ilisema Idara ya Mawasiliano ya Mudavadi kwenye taarifa
“Mikataba hii itaimarisha azma ya Kenya na Hungary kukuza ushirikiano wa pande mbili juu ya mabadilishano ya utaalam na mienendo bora ya kilimo ili kuboresha uzalishaji wa kilimo katika nchi zetu zote.”
Wakati wa ziara hiyo ya siku tatu, Muavadi pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Hungary Dkt. Tama Sulyok.
Hungary ni mshirika muhimu wa Kenya katika sekta za kilimo na elimu na hutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 200 wa Kenya kila mwaka.