Kenya na Ghana zimetia saini mikataba saba ya maelewano, kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais William Ruto, alisema mikataba hiyo ikiwa ni pamoja na ile iliyotiwa saini na washirika wa kibiashara kutoka Kenya na Ghana, inanuia kufanikisha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Kulingana na Rais Ruto, lengo la mikataba hiyo ni kupanua fursa za kibiashara, sekta ya kibinafsi pamoja na kuwawezesha raia wa nchi hizo mbili.
Mikataba hiyo ilijumuisha ushirikiano katika sayansi na teknolojia, utalii, elimu, uongozi na ulinzi.
“Wakati wa mashauriano na Rais Nana Akufo-Addo, tumetambua kwamba mikataba hii yana umuhimu katika ukuaji wa uhusiano wa kidiplomasia,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto aliyasema hayo wakati wa mkutano na wanahabari katika afisi ya Rais Nana Akufo-Addo, baada ya mkutano wa viongozi hao wawili.