Kenya na Ethiopia zimetia saini mikataba saba ambayo itaimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Mikataba hiyo ilisainiwa wakati wa mapokezi ya waziri mkuu wa Ethiopia humu nchini, Abiy Ahmed na mwalishi wake rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi.
Viongozi hao wawili walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja za biashara na uwekezaji, kilimo, uvuvi, uchukuzi, teknolojia ya mawasiliano, utalii, afya, utamaduni na uhifadhi wa misitu, mbali na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha amani na uthabiti katika eneo la upembe wa Afrika.
Na ili kuimarisha zaidi uhusiano baina ya raia wa nchi zote mbili, viongozi hao walikubaliana kuchukua hatua za kukuza mwingiliano huku Kenya ikidhihirisha uamuzi huo wiki chache zilizopita kwa kuondoa hitaji la kibali cha usafiri kwa raia wa Ethiopia wanaoingia humu nchini.
Wakikariri kujitolea kwao kwa ajili ya kuleta amani na udhabiti katika eneo la upembe wa Afrika, Rais Ruto na waziri mkuu Ahmed walithibitisha kujitolea kwao kutambua, kuheshimu na kudumisha uhuru na hadhi ya nchi hizo pamoja na kutoruhusu mabadiliko ya uongozi yalio kinyume cha katiba ya serikali pamoja na kujihusisha kwenye masuala ya kisiasa ya nchi za bara Afrika dhidi ya mataifa mengine.
Viongozi hao baadaye walizuru kituo kidogo cha Suswa kilichoko kaunti ya Kajiado ambacho husambaza umeme kwa Kenya na Ethiopia.