Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya, leo Alhamisi alikuwa mwenyeji wa balozi wa Uchina hapa nchini Guo Haiyan, katika makao makuu ya wizara ya Ulinzi Jijini Nairobi.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kati ya Soipan na Guo, ulilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta kuu muhimu kwa lengo la kuweka imara uwezo wa kiusalama.
Mazungumzo kati ya wawili hao, yaliangazia haja ya kushirikiana katika sekta za usalama kuambatana na hatari zinazochipuza ulimwenguni, kama vile ugaidi, uhalifu wa mtandaoni na uhalifu wa kimataifa.
“Tuliangazia mbinu za kupanua ushirikiano wa ulinzi kati ya Kenya na China, ili kujumuisha changamoto ibuka,” alisema Waziri Soipan baada ya mkutano huo.
Alisema Beijing inasalia kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Kenya.
“Raia wa Kenya na wale wa Jamhuri ya watu wa China, wanafurahia uhusiano dhabiti wa pande mbili kuhusu diplomasia, uchumi, utamaduni na uhusiano baina ya watu,” aliongeza Soipan.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mkuu wa Vikosi vya Ulinishow hapa nchini Jenerali Charles Muriu Kahariri miongoni mwa maafisa wakuu wa KDF.