Baraza Kuu la Mfuko wa Uhaianuai wa Kunming kwenye Mkutano wa Uhaianuai wa COP16 wa Umoja wa Mataifa 2024 umepitia upya na kupitisha miradi midogo katika mabara sita inayounga mkono nchi 15 zinazoendelea.
Mfuko wa Uhaianuai wa Kunming ulianzishwa mwaka 2021 wakati wa mkutano wa COP15. Wakati huo, Rais wa China Xi Jingping alitangaza wakati wa mkutano wa uongozi wa viongozi wakuu kutolewa kwa yuan bilioni 1.5 za kuanzisha Mfuko wa Kunming kuziunga mkono nchi zinazoendelea.
Baada ya kuupitia upya, Baraza Kuu la Mfuko wa Uhaianuai wa Kunming kwenye mkutano wa COP16 likiongozwa na Inger Andersen, Mkurugenzi Mkuu wa UNEP, Huang Runqiu, Waziri wa Mazingira na Ikolojia wa China na Astrid Schomaker, Katibu Mkuu wa CBD limetoa wito kwa wanufaikaji wa mfuko huo kutumia mfuko huo kuboresha uhaianuai pamoja na kuangazia malengo muhimu ya Mpangokazi wa Uhaianuai Duniani wa Kunming Montreal.
Mfuko huo ulitangazwa Oktoba 25, 2024 wakati wa mkutano wa COP16 mjini Cali nchini Colombia.
Wakati wa kutangazwa kwa mfuko huo, Waziri wa Mazingira na Ikolojia wa China Huang Runqiu alisema, “tunatumai kuwa pande husika zitatumia fursa ya Mfuko wa Kunming kuboresha ulinzi wa uhaianuai, kujenga jamii ya wanadamu, na kuangazia malengo muhimu ili kusaidia kuboresha ulinzi na pia kuendeleza ajenda ya mwaka 20230 na mpangokazi wa Kunming.”
Mfuko huo unalenga kuunga mkono teknolojia, uwezo na ushirikiano wa pande nyingi.
Miradi hiyo midogo inajumuisha: mmoja kutoka Ulaya ya Kati, 4 kutoka Asia Pasifiki, 2 kutoka Afrika na 2 kutoka Amerika Kusini. Hii inajumuisha mabara sita na jumla ya nchi 15 ambazo ni pamoja na Kenya, Salvador, Guatemala, Honduras, Bogdan, Chile na Papua New Guinea.
Nchi zingine ni Nepal, Malawi, Namibia, Trinidad and Tobago, Samoa, Albania, Ethiopia na Madagascar.
Taasisi zinazosimamia utekelezaji wake ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).
(Taarifa hii ilitayarishwa kama sehemu ya Ushirika wa 2024 CBD COP16 ulioratibiwa na Mtandao wa Earth Journalism wa shirika la Internews.)