Kamati ya Ushirikiano wa Vyama vya Kisiasa, PPLC imetoa wito wa kufanywa kwa majadiliano ili kumaliza mivutano ya kisiasa nchini.
PPLC inasema ubabe wa kisiasa unaoshuhudiwa kati ya serikali ya Kenya Kwanza na upande wa upinzani unaweza ukasababisha machafuko nchini.
Wito wa kamati hiyo unakuja wakati serikali ikionya kuwa haitaruhusu kufanyika kwa maandamano nchini siku za Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki hii.
Aidha serikali imeapa kukabiliana vilivyo na yeyote atakayesababisha vurugu na uharibifu wa mali ya umma na kibinafsi kama ilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano yaliyofanyika wiki jana.
Muungano wa Azimio unashikilia kuwa maandamano hayo yataendelea mbele kama ilivyopangwa ili kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha na kubatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023.
Viongozi wa kidini wanasema wako radhi kupatanisha serikali na upande wa upinzani, wakionya kuwa mivutano inayoshuhudiwa ya kisiasa kati ya pande mbili ni hatari kwa nchi.