Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Daktari Alfred Mutua amesema Kenya imejitolea kutuma maafisa wake wa polisi wapatao 1000 nchini Haiti wakasaidie kutoa mafunzo kwa polisi wa huko, na kuwasaidia kurejesha utulivu kando na kulinda asasi muhimu.
Kupitia Twitter Waziri Mutua alisema Kenya inasimama na watu wa asili ya Afrika kote ulimwenguni, wakiwemo wale wa eneo la Caribbean, hatua inayowiana na sera za kigeni za umoja wa Afrika na za Kenya kuhusu uafrika na katika tukio hili, kurejesha kuvuka kwa bahari ya Atlantic.
Kenya itatuma polisi hao nchini Haiti punde baada ya kupokea idhini kutoka kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa na kukamilisha mahitaji ya sheria za Kenya.
Shughuli ya kutathmini mpango huo inapangiwa kutekelezwa na jopo kutoka kitengo cha polisi katika muda wa majuma machache yajayo. Utathmini huo utatoa mwongozo kuhusu idhini na mahitaji ya kikazi ya hatua hiyo.
Waziri Mutua alisisitiza pia, kujitolea kwa Kenya kusimama na nchi nyingine za Afrika ili kuzisaidia kuafikia amani na udhabiti zikiwemo Sudan, DRC na Niger.