Kenya inatarajiwa kutumia mashindano ya The Prefontaine Classic Diamond League, yatakayoandaliwa nchini Marekani Jumamosi usiku kuchagua washiriki wa mbio za mita 10,000 katika michezo ya Olimpiki.
Kwa jumla Kenya imewatuma wanariadha 28 wanawake 13 na wanaume 15 kuwania muda wa kufuzu kwa michezo ya Olimpiki, itakayoandaliwa jijini Paris Ufaransa kati ya Julai 26 na Agosti 11 mwaka huu.
Fainali ya mita 10,000 wanawake inatarajiwa kuwa na msisimko wa kipekee ikimsirikisha bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za nyika Beatrice Chebet,mshindi wa mbio za nyika za Sirikwa Classic Emmaculate Achol Anyango na Grace Loibach Nawowuna wakiwania kutimiza muda wa dakika 30 na sekunde 40 unaohitajika ili kufuzu kwa Olimpiki.
Wengine watakaoshiriki mbio hizo ni Lillian Kasait,Agnes Jebet Ngetich ,Margaret Chelimo,Janeth Chepnetich,Cintia Chepng’eno,Diana Chepkori,Faith Cherotich,Loice Chemnung,Jesca Chelang’at,Mirriam Chebet,Selah Busienei na Catherine Reline Amanang’ole.
Katika fainali ya wanaume mshindi wa nishani ya fedha ya dunia mwaka jana Daniel Simiu Ebenyo,Samwel Chebolei na Benson Kiplangat watapambana wakilenga kutimiza muda wa kufuzu wa dakika 27.
Washiriki wengine katika fainali ya wanaume kesho usiku ni Kibiwott Kandie,Peter Mwaniki,Nicholas Kipkorir,Benard Koech,Edwin Kurgat,Ronald Kwemoi,Weldon Langat,Daniel Mateiko,Stanley Waithaka na Gideon Rono.