Kenya inatarajia kupata mkopo wa shilingi bilioni 152 kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani, IMF. Hatua hii inafuatia kukamilika kwa mazungumzo ya awamu ya sita ya kutathmini ustahiki wa Kenya kuongezewa mkopo.
Shirika la IMF limesema litasambaza shilingi bilioni 100.8 chini ya mkataba wa kuiongezea Kenya ruzuku na kisha shilingi bilioni 419.9.
Mkopo huo unatarajia kusaidia kudhibiti hali ya kiuchumi kutokana na sera thabiti za kupunguza kiwango cha gharama ya maisha, ushirikishaji mikakati ya kifedha na ulipaji madeni.
Bodi ya IMF inabashiri uchumi wa taifa hili kukua kwa asilimia tano mwaka huu kutokana na uongozi bora, ubunifu wa nafasi za ajira, utekelezaji wa mikakati ya mapato kwa kupanua kiwango cha ukusanyaji ushuru, kuimarika kwa ushindani wa kuuza bidhaa za humu nchini katika mataifa ya kigeni pamoja na usimamizi wa fedha za umma katika mashirika ya serikali.
Bodi hiyo pia limesisitiza umuhimu wa ushirikishaji mikakati ya kifedha iwapo taifa hili litakabili mzigo wa ulipaji madeni, hatua itakayosaidia nchi hii kuafikia kiwango kipya cha kupata mkopo wa asilimia 55 ya pato jumla ifikapo mwaka 2029.
Kenya pia inatarajia kupata shilingi bilioni 9.7 za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Bodi ya IMF imekariri kwamba kiwango cha kubadilishana sarafu kinapaswa kubadilika kuambatana na hali ya soko duniani.