Kenya kupokea helikopta 16 kutoka kwa serikali ya Marekani kufikia mwaka 2025

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto na mwenyeji wake Rais Joe Biden wa Marekani, katika Ikulu ya White House.

Kenya inatarajiwa kupokea helikopta 16 zilizotengenezewa Marekani nane zikiwa aina ya Hueys na nane aina ya MD-500s kati ya mwaka 2024 na 2025, kulingana na serikali ya Marekani.

Kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizo mbili, hasaa katika sekta ya afya, Marekani itatoa helikopta hizo kuimarisha usalama na amani ya kanda hii na pia kushiriki katika mipango ya kulinda amani.

Hayo yalijiri baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuwa mwenyeji wa Rais William Ruto katika ikulu ya White House leo Alhamisi, Washington D.C.

Katika mkutano huo, viongozi hao wawili walijadili wa kina kuhusu demokrasia, haki za kibinadamu na uongozi, ushirikiano katika sekta ya afya, biashara na uwekezaji, ushirikiano baina ya watu, dijitali, ushirikiano wa kiteknolojia, amani na usalama miongoni mwa maswala mengine.

Ili kuunga mkono amani na salama wa taifa hili, serikali ya Marekani ilisema kuwa ushirikiano wa nchi hizo mbili unajumuisha mazungumzo kuhusu amani, kulinda amani katika ngazi za kimataifa, uongozi katika sekta ya usalama, maswala ya wakimbizi na ushirikiano katika usalama wa kimtandao.

“Ushirikiano wa Marekani na Kenya unatekeleza jukumu muhimu katika juhudi za kimataifa za kushinda vita  Al-Shabaab na ISIS, ambazo zimekita mizizi Afrika Mashariki pamoja na makundi mengine ya kigaidi ya Kimataifa,” ilisema taarifa hiyo.

Kuhusu vita dhidi ya ugaidi, nchi hizo mbili zinatarajiwa kutia saini mkataba wa maelewano kuhusu kupanua uwanja wa ndege wa Manda Bay.

Serikali ya Marekani ilisema upanuzi wa uwanja huo, utawezesha Kenya kuwa na miundomsingi inayohitaji kuongeza operesheni zake dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabab.

Aidha serikali hiyo ya Marekani, imesema kuwa itaunga mkono juhudi za Kenya za kuwapeleka maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti, kusaidia taifa hilo la kusini mwa Caribbean kurejesha utulivu na udhabiti.

Share This Article