Timu ya taifa ya soka ya Kenya-Harambee Stars, itashuka uwanjani Bingu mjini Lilongwe nchini Malawi leo alasiri kwa mechi ya tatu ya kundi F kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Burundi.
Pambano hilo litang’oa nanga saa kumi kamili, Kenya ikilenga ushindi wa pili baada ya kuititiga Ushelisheli mabao matano kwa bila katika mechi ya pili mwezi Novemba mwaka jana.
Kocha wa Kenya Engine Firat ana imani ya vijana wake kusajili ushindi licha ya kuchezea mechi hiyo katika taifa la kigeni.
“Tunapambana na timu iliyo na wachezaji wenye kasi na tumejiandaa kisaikojolia kukabiliana nao. Lengo letu ni kujaribu kila hali kupata alama tatu,” alisema Firat.
Kwa upande wake, nahodha wa Harambetatu Stars Michael Olunga anasema watajitahidi kuafikia matokeo bora.
Olunga alisema, “Tumekuwa tujiandaa vyema, wachezaji wote wanahisi vizuri na tuna matumaini kila mchezaji atacheza vizuri na tutapata ushindi.”
Naye kocha wa Burundi Etien Ndayiragije amesema wamajiandaa vyema kukabiliana na majirani Kenya leo jioni.
“Hali iko shwari, wachezaji wangu wana nia na wana njaa ya kupeform ili tupate matokeo, mpinzani wetu Kenya tumekaa tumemsoma vizuri, “akasema Ndayiragije.
Timu zote mbili zina alama sawa tatu huku atakayeshinda leo akiweka hai matumaini ya kufuzu.
Mchuano wa leo utakuwa wa sita wa kimataifa kati ya Kenya na Burundi, Kenya ikishinda mechi mbili, Burundi moja na kusajili sare mbili.
Runinga ya taifa KBC Channel 1 na Idhaa zote za redio za KBC zitarusha mubashara mchuano huo.
Baada ya pambano la leo, Kenya watasalia nchini Malawi ambapo watawaalika mabingwa wa Afrika, Ivory Coast Jumanne ijayo.
Katika mchuano mwingine wa kundi hilo leo usiku, Ivory Coast itawaalika viongozi wenza wa kundi F Gabon mjini Abijan.
Gambia itakuwa mwenyeji wa Ushelisheli katika mechi nyingine ya mzunguko wa tatu kundini F.
Timu itakayoongoza kundi hilo itafuzu moja kwa moja kwa kipute cha Kombe la Dunia mwaka 2026, ambacho kitaandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Marekani, Canada na Mexico.