Kenya kufutilia mbali hitaji la viza kwa raia wa Comoros

Martin Mwanje
2 Min Read

Kenya imeelezea dhamira yake ya kufutilia mbali hitaji la viza kabla ya mwisho wa mwaka huu kwa watu wote walio na nyaraka halali za usafiri zilizotolewa na Umoja wa Comoros wanaoingia humu nchini. 

Hayo yamesemwa na Rais William Ruto ambaye yupo nchini Comoros kuhudhuria maadhimisho ya miaka 48 ya Siku ya Uhuru wa nchi hiyo.

Ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Ruto alisema Kenya inafanya kazi kwa karibu kuwaruhusu wanafunzi kutoka nchini Comoros kusomea masomo ya juu humu nchini na kulipa karo sawia na wanafunzi Wakenya.

“Kenya inasimama na Comoros kama mshirika wa kimaendeleo, ikijitolea kuimarisha ushirikiano wetu kwa manufaa ya watu wetu. Kwa pamoja, tunaweza tukatumia uwezo wetu kubuni nafasi, kukuza ubunifu, na kujenga chumi endelevu zisizomwacha yeyote nyuma,” alisema Rais Ruto.

Ruto alimpongeza Rais Azari Assoumani kwa kuridhia kuchukua wajibu wa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU mwaka huu akisema Comoros ni kisiwa cha kwanza kuchukua uongozi wa umoja huo.

Kulingana naye, hatua hiyo itawatia imani watu wote wa bara la Afrika haijalishi ni nchi gani wanakotoka, ndogo au kubwa.

Rais alisisitiza dhamira ya Kenya kuiunga mkono Comoros wakati mwenzake Azari akiongoza umoja huo kufikia mafanikio makubwa na kuzishughulikia changamoto zinazowakabili watu kila siku.

Ruto alisema anatazamia hatua kubwa kupigwa katika kuifanyia AU mabadiliko ya kitaasisi ambayo yatawezesha Tume ya AU, taasisi za AU na taasisi maalum kufikia uwezo wao kikamilifu na kutimiza wajibu wao wa kuwezesha kuchipuka kwa umoja ambao unaweza ukashiriki ipasavyo masuala ya dunia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *