Rais William Ruto amesema Kenya itashirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE ili kufanya Mkutano wa 28 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu kuwa wenye manufaa kwa wote.
Ruto amesema mikutano ya awali ya tabia nchi itakayofanyika katika miji ya Paris na Nairobi ni sharti isaidie kuandaa makubaliano yatakayokubaliwa na wote: Nchi zilizoendelea na zinazoendelea, nchi zinazozalisha gesi chafuzi kwa mazingira na zisizozalisha gesi chafuzi, wakati wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa COP28 mjini Dubai.
“Mabadiliko ya tabia nchi ni tishio linalotukabili sisi sote na hakuna wakati wa kulaumiana na sarakasi. Tunatazamia mkutano wa COP28 kutoa mwelekeo mpya katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.”
Rais aliyasema hayo alipokutana na Waziri wa Viwanda na Vyama vya Ushirika wa UAE Dr. Sultan Al-Jebr ambaye amepangiwa kuchukua urais wa COP28.
Dr. Al-Jebr alisema umoja wakati wa mkutano wa COP28 utatoa suluhisho mwafaka na “kufanya wa COP28 kuwa wa kuleta mabadiliko”.
Alisema UAE inatafuta kuwekeza katika rasilimali za nishati mbadala za Kenya.
Rais Ruto alipongeza ushirikiano uliopo kati ya Kenya na UAE, hasa makubaliano ya mafuta kati ya serikali za nchi hizo mbili.