Kenya imeshinda ombi la kuwa mwandalizi wa kongamano maalum la Transform Afrika mwaka 2024.
Tangazo hilo lilifanywa wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Mobile World Congress (MWC) jijini Barcelona nchini Uhispania.
Kwenye hotuba yake ya kukubali maandalizi ya kongamano hilo, waziri wa habari na teknolojia ya mawasiliano Eliud Owalo alidokeza kuwa ushindi huo wa kuandaa kongamano hilo ni ishara ya uwezo wa Kenya kwenye maswala ya habari na teknolojia ya mawasiliano na kama taifa linaoongoza katika kanda hii kwenye mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano kuhusu ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Kongamano la Transform Africa, ambalo huandaliwa kila mwaka na kampuni ya The Smart Africa Alliance, ndilo tajika barani Afrika kwa kuunganisha viongozi wa sekta ya teknolojia ya mawasiliano wa serikali za mataifa, wafanya biashara na mashirika ya kimataifa kutoka sio tu barani afrika bali ulimwenguni kote.
Ushirikiano huo unalenga kubuni mbinu bunifu za kuunda, kudumisha na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali barani Afrika. Kongamano hilo litaandaliwa jijini Nairobi kati ya tarehe 28 na 30 mwezi Agosti mwaka huu.