Kenya itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Maonyesho ya Afya Duniani litakaloandaliwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Kongamano hilo litakaloandaliwa na shirika la Informa Markets litakuwa la kwanza kubwa kuandaliwa Afrika Mashariki.
“Tukio hili litatoa fursa ya Kenya kunadi fursa za uwekezaji na maendeleo katika teknolojia ya tiba,” amesema Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni.
“Kutokana na hali inayobadilika ya magonjwa duniani na maendeleo ya kasi ya teknolojia, kongamano hilo litaleta pamoja wataalam kutoka sekta za biashara, wanataaluma, na wasomi ili kukuza uhamishaji wa maarifa, ushirikiano wa kimkakati na uwekezaji katika afya.”
Katibu Muthoni anasema kongamano hilo linawiana na ajenda ya Kenya ya kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote na hivyo kupiga jeki nafasi ya nchi hii kama kinara katika uvumbuzi na uwekezaji wa afya barani Afrika.
“Litatoa fursa za ushirikiano kwa washikadau wa ndani na nje ya nchi na hivyo kuifanya Kenya kuwa kituo cha afya cha kikanda,” aliongeza Muthoni.
Aliyasema hayo leo Jumatatu alipokutana na Tom Coleman, Mkurugenzi wa Portfolio katika shirika la Informa Markets ili kujadili maandalizi ya kongamano hilo.