Kenya kushughulikia changamoto za kibiashara zinazokumba EAC

Tom Mathinji
2 Min Read

Kenya itatekeleza wajibu wake kushughulikia changamoto zinazokumba mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ili kufanikisha uchukuzi wa binadamu, bidhaa na utoaji huduma katika kanda hiyo.

Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Maeneo Kame Beatrice Askul amesema wizara yake inajizatiti kushughulikia changamoto za mpakani, zinazohujumu usafirishaji shwari wa bidhaa na huduma katika kanda hii.

Amesema Kenya inaendelea kuimarisha uhusiano wake na mataifa wananchama wa EAC ili kuharakisha ufanisi wa biashara za mipakani, ubadilishanaji ujuzi na utangamano.

Waziri aliyasema hayo jana Alhamisi alipoanzisha safari ya awamu ya saba ya waendeshaji baisikeli afisini mwake, inayowaleta washiriki kutoka mataifa sita ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Safari hiyo ya kilomita 6,000 ya uendeshaji baisikeli ambayo huandaliwa kila mwaka, ilianza Agosti 1, 2024 mjini Bunjumbura nchini Burundi huku waendeshaji hao wakiwasili hapa nchini Agosti 17,2024.

Waziri huyo alisema hafla hiyo ya uendeshaji baisikeli hupiga jeki mchakato wa utangamano kupitia uhamasishaji, utalii wa kimazingira, ukuaji wa uchumi, usalama wa chakula na afya miongoni mwa maswala mengine.

“Hafla hiyo itaimarisha utangamano EAC kushughulikia ajenda zake, ikiwa ni pamoja na amani, utalii, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi na umoja,” alisema Waziri Askul.

Mataifa sita yanayoshiriki hafla hiyo ya uendeshaji baisikeli ni pamoja Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Tanzania, na Uganda.

Share This Article