Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zina sheria zinazoharamisha mahusiano ya kimapenzi kati ya watu wa jinsia moja, lakini bado haijatekeleza sheria hizo.
Haya yalisemwa kwenye kikao cha kamati ya bunge la taifa kuhusu utekelezaji.
Katibu wa utangazaji Edward Kisiang’ani, aliambia kamati hiyo kwamba kuenea kwa ajenda ya ndoa kati ya watu wa jinsia moja nchini kunaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watu.
Hatua hiyo anasema itafanikisha ajenda ya ung’ang’aniaji wa rasilimali za bara hili la Africa.
“Hili ni shambulio dhidi ya utamaduni wa Kiafrika. Kuna ajenda kwamba idadi ya watu wa Afrika isiongezeke ili rasilimali za Afrika ziweze kuchukuliwa na watu wengine.” Alisema Kisiangani.
Kulingana naye mpango huo ni wa muda mrefu na kwamba kwa mtazamo wa uchumi wa kisiasa falsafa hiyo inalenga kuikalia tena Afrika.
Joseph Mogosi Motari Katibu wa utunzaji wa jamii aliifahamisha Kamati hiyo kuwa serikali imeboresha ustawi wa watoto nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia na Kukabiliana na Unyanyasaji dhidi ya Watoto mwaka 2019 hadi 2023.
Wanachama wa kamati hiyo hata hivyo hawakuridhishwa na majibu waliyopatiwa wakiyataja kuwa ya jumla mno na kwamba hawakugusia kiini cha suala hilo kama lilivyoulizwa kwenye mjadala bungeni.
Mbunge Mark Mwenje alisema kwamba hata ingawa watatunga sheria za kuharamisha mahusiano ya jinsia moja, mashirika ya kimataifa ya misaada huenda yakamshurutisha Rais kutoitia saini.
“Tuna mashirika yasiyo ya kiserikali yanayokuza masuala ya wapenzi wa jinsia moja, Wizara inafanya nini kuhusu NGOs hizi kwa sababu kufikia sasa, ulipaswa kufanya mkutano wa pande zote na mashirika hayo, vyombo vya habari na wadau kwa sababu huo ndio mwelekeo tunaochukua” aliuliza Mwenje.
Kamati hiyo ya utekelezaji ya bunge ilialika maafisa wa wizara ya Mawasiliano, Wizara ya leba na Ustawi wa Jamii na Mwanasheria Mkuu kuelezea kuhusu hali ya utekelezaji wa Hoja ya mbunge wa Nyali Mohamed Ali.
Ali anataka iwe marufuku kujadili, kuchapisha na kusambaza habari zinazokuza mahusiano ya watu wa jinsia moja nchini.