Kenya Airways yarejesha safari za moja kwa moja kati ya Nairobi na Mogadishu

Marion Bosire
2 Min Read
Ndege ya shirika la Kenya Airways.

Safari za moja kwa moja za ndege za kampuni ya Kenya Airways kati ya Nairobi nchini Kenya na jiji la Mogadishu nchini Somalia zimerejelewa leo, Februari 15, 2024.

Hii ni baada ya kusitishwa kwa muda mwaka 2020 kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa Corona, janga lililokumba ulimwengu mzima.

Meneja wa mauzo na huduma kwa wateja katika kampuni ya Kenya Airways Julius Thairu, alitangaza kurejelewa kwa safari hizo jana.

Kutakuwa na safari tatu kila wiki, Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi saa nane alasiri na safari ya kurejea kutoka Mogadishu itakuwa ikianza saa kumi na dakika 35 jioni.

Mipango ya kurejelewa kwa safari hizi ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwezi Novemba mwaka jana ambapo meneja Thairu alisema hatua hiyo ilichochewa na ongezeko la biashara na safari za ndege kati ya Kenya na Somalia.

Kulingana na Thairu mipango hiyo ni sehemu ya mikakati ya Kenya Airways ya kupanua wigo wa huduma zao kwa lengo la kuunganisha sehemu mbali mbali za bara Afrika na hatimaye kuchangia katika shughuli za kiuchumi barani humu.

Kenya na Somalia zilitia saini mkataba wa pande mbili wa huduma za usafiri wa angani na hivyo kuimarisha pakubwa huduma za kampuni ya Kenya Airways.

Share This Article