Mkuu wa vikosi vya ulinzi hapa nchini Jenerali Charles Kahariri ametoa shukrani kwa serikali ya Japani kwa kusaidia Kenya kutoa mafunzo kuhusu amani katika kituo cha mafunzo kuhusu amani cha Karen, jijini Nairobi.
Akizungumza baada ya kuwa mwenyeji wa Balozi wa Japani hapa nchini Okaniwa Ken katika makao makuu ya vikosi vya ulinzi, Kahariri alidokeza kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano mwema tangu miaka ya 60.
Jenerali huyo aliongeza kuwa kupitia mchango wake katika sera ya amani, Japan imeshiriki vilivyo katika kudumisha amani duniani kupitia sheria za amani na usalama.
Kupitia Shirika la Ushirikiano wa kimataifa la Japani (JICA), Kenya imetekeleza miradi kadhaa ya maendeleo kama vile eneo maalum la kiuchumi la Dongo Kundu, upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi, bandari ya Mombasa, pamoja na ujenzi wa madaraja ya Nyali, Mtwapa na Kilifi.
Kwa upande wake, Balozi Ken alielezea thamani ya uhusiano kati ya Kenya na Japani, akidokeza kuwa anatazamia kuimarishwa kwa uhusiano wa kijeshi ulioanzishwa.
Maeneo ambapo kenya na Japani zinalenga kushirikiana ni pamoja na usalama wa baharini, mazoezi ya pamoja ya kijeshi na ukabilianaji na majanga.