KCAA yasema Adani haihusiki katika upanuzi wa JKIA

Marion Bosire
1 Min Read

Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini, KAA imefafanua kuhusu taarifa iliyochapishwa na gazeti moja la humu nchini kwamba kampuni ya Adani inahusika na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Katika taarifa, kaimu mkurugenzi mkuu wa KAA Dkt. Mohamud Gedi alithibitisha kwamba pendekezo la awali la Adani kutekeleza kazi hiyo lilifutiliwa mbali.

Gedi alisisitiza kwamba kamwe hakuna mazungumzo ya aina yoyote yanayoendelea kati ya KAA na kampuni ya Adani au washirika wake kuhusu uwanja wa JKIA.

“Mradi wa upanuzi wa JKIA unafadhiliwa na serikali ya Kenya na unatekelezwa kulingana na sera na michakato iliyowekwa ya sekta ya umma,” aliendelea kusema Gedi katika taarifa hiyo.

Alimalizia kwa kuhakikishia umma kwamba mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege nchini imejitolea kwa uwazi na itahakikisha kwamba wadau na umma wanapokea habari ifaavyo.

Taarifa hiyo ya gazeti ilikuwa imedai kwamba kampuni ya Adani iliyokataliwa awali bado inahusika kwenye mradi huo muhimu.

Mwaka 2024, habari za uhusika wa Adani katika mradi huo zilizua tumbo joto kiasi cha wafanyakazi wa uwanja huo wa ndege wa JKIA kugoma kwa kuhofia usalama wa ajira zao.

Hali hiyo ilisababisha kutupiliwa mbali kabisa kwa mpango huo wa Adani kukarabati JKIA.

Share This Article