Kawira apata Mwangaza mahakamani

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Saa chache baada ya bunge la Seneti kumbandua Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, Mahakama Kuu imempa Gavana huyo sababu ya kutabasamu baada ya kufutilia mbali hatua hiyo.

Kupitia kwa wakili wake Eliud Mutuma, Mwangaza alifika mahakamani leo Jumatano kupinga hatua ya bunge la Seneti kudumisha kutimuliwa kwake na bunge la kaunti ya Meru.

Huku akifutilia mbali kutimuliwa kwa Mwangaza, Jaji Bahati Mwamuye wakati huo huo alitoa agizo la kumzuia spika wa bunge la Seneti kuchapisha kwenye gazeti rasmi la serikali ilani ya kutangaza wadhifa wa Gavana wa kaunti ya Meru kuwa wazi.

Kesi hiyo iliyowasilishwa na Mwangaza inatarajiwa kusikilizwa Septemba 17, 2024.

Jana Jumanne usiku, bunge la Seneti lilipiga kura kudumisha uamuzi wa bunge la kaunti ya Meru kumtimua Gavana Mwangaza.

Mashtaka yaliyolimbikiziwa Mwangaza na bunge la kaunti ya Meru ni pamoja na ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlaka na utovu wa maadili.

Katika shtaka la kwanza la ukiukaji katiba, Maseneta 26 walipiga kura kuwa Mwangaza ana hatia huku wanne wakisema hana hatia. Maseneta 14 hawakupiga kura.

Katika shtaka la pili la utovu wa maadili, Maseneta 26 walisema ana hatia na wanne kusema hana hatia.

Na katika kosa la tatu la utumizi mbaya wa mamlaka, Maseneta 27 walipiga kura kusema ana hatia na Seneta mmoja kupiga kura kupinga kosa hilo.

“Kuambatana na sura ya 181 ya katiba, sehemu ya 33 ya serikali za kaunti na kanuni za bunge nambari 86 ya bunge la Seneti, bunge la Seneti limeazimia kumuondoa mamlakani Gavana wa Meru Kawira Mwangaza,” alitangaza spika wa bunge hilo Amason Kingi.

Mwangaza ambaye alihudhuria vikao vya bunge hilo vya kusikiliza mashtaka dhidi yake, alikuwa amekanusha mashtaka hayo yaliyowasilishwa na bunge la kaunti ya Meru.

Awali, Gavana huyo alinusurika majaribio mawili ya kumuondoa mamlakani, jaribio la kwanza likiwa mwezi Disemba mwaka 2022 na la pili likiwa mwezi Novemba mwaka 2023.

Share This Article