Serikali ya kaunti ya Wajir imezindua juhudi za dharua za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa hatari wa Kala-azar, ambao husababishwa na viini vya Leishmania.
Tayari watu 18 wamefariki kutokana na ugonjwa huo huku wengine zaidi ya 500 wakiambukizwa ugonjwa huo katika muda wa miezi mitatu iliyopita, huku maambukizi hayo yakiendelea kuenea.
Maafisa wa afya kwenye kaunti hiyo wanajitahidi kukabiliana na maambukizi hayo yaliyoanza mwezi Disemba mwaka jana, huku watu 106 wakiendelea kupokea matibabu hospitalini.
Maafisa wa matibabu wamethibitisha visa 532 vya ugonjwa huo wa Kala-azar kufikia sasa.
Naibu wa Gavana wa kaunti hiyo Ahmed Muhumed, amesema kaunti hiyo imeweka mikakati ya kukabili maambukizi hayo.
Maafisa wa afya wameonya kuwa hali hiyo huenda ikazorota zaidi endapo wakazi walio na dalili za ugonjwa huo hawatapata matibabu ya haraka.
Kaunti hiyo imetoa wito kwa washirika na serikali ya kitaifa kusaidia katika juhudi za kuzuia maambukizi hayo.
Baadhi ya dalili za ugonjwa huo wa Kala-Azar ni pamoja na kupunguka kwa uzani wa mwili, joto mwilini,kuharisha,uchovu na ngozi kuwa nyeusi zaidi.