Kaunti ya Samburu yaangaziwa kisa ukaguzi wa hesabu

Maafisa wakuu wa serikali ya kaunti ya Samburu walikosa kuwasilisha ripoti za ukaguzi wa hesabu wa matumizi ya fedha mwaka 2024/2025.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya kaunti ya Samburu imejipata matatani kufuatia maswali kuhusu ripoti za ukaguzi wa hesabu wa matumizi ya pesa za umma.

Gavana wa kaunti hiyo Lati Lelelit alifika mbele ya kamati ya uwekezaji wa pesa za umma ya bunge la Seneti leo kwa mara ya kwanza kabisa, baada ya kususia miito ya kamati hiyo mara kadhaa.

Kamati hiyo imekuwa ikimsaka Lelelit kuhusiana na maswali ya matumizi ya fedha za kaunti hiyo mwaka 2024/2025.

Gavana huyo na maafisa wakuu wa serikali ya kaunti ya Samburu walikosa kuwasilisha ripoti za ukaguzi wa hesabu wa matumizi ya fedha katika kipindi hicho.

Wakiwa pamoja na maafisa wa kampuni ya maji ya Samburu, wote hao wako katika hatari ya kutozwa faini ya shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitatu gerezani. Hii ni iwapo watapatikana na hatia ya kukiuka sheria ya usimamizi wa fedha za umma.

Maseneta walitaka pia kupata ufafanuzi kuhusu jinsi shilingi milioni 68, zilizotengewa ununuzi wa vifaa vya kuboresha upatikanaji wa maji zilipotea.

Kikao cha kamati hiyo kilipamba moto huku Maseneta wakisema ukaguzi wa mkaguzi mkuu wa hesabu uligundua uwezekano wa makosa makubwa ya kifedha katika kaunti ya Samburu.

Share This Article