Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga leo Jumatatu ameagiza Bodi ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha ya kaunti hiyo kusimamisha mishahara ya madaktari 59 wanaoshiriki mgomo wa kitaifa, ulioitishwa na chama cha madaktari nchini, KMPDU.
Akiwahutubia wanahabari afisini mwake, Kahiga alisema serikali ya kaunti hiyo haitawalipa mishahara madaktari hao kwa sababu wamekiuka sera ya ajira ya kaunti hiyo, kwa kuwa wao ni wafanyakazi wa kaunti na wala sio wafanyakazi wa serikali kuu.
“Leo nimeagiza Bodi ya PSC na Wizara ya Fedha ya kaunti kusimamisha mishahara ya madaktari 59. Tuliwaandikia barua kwa nini hatua za kinidhamu zisichukuliwe dhidi yao, lakini hawakujibu,” alisema Gavana Kahiga.
Aliwalaumu madaktari hao akisema kuwa, badala ya kushiriki mgomo, wangejadiliana na serikali za kaunti ambazo zimewaajiri.
“Mgomo huu sio halali, madaktari wameajiriwa na kaunti, kwa hivyo hakuna vile chama chao kitajadiliana na serikali kuu, ila kinapaswa kujadiliana na serikali zote 47 za kaunti,” alidokeza Kahiga.
Mgomo wa kitaifa wa madaktari umeingia siku ya 25 leo Jumatatu huku Wakenya wengi wakiendelea kutatizika kupata huduma za afya.