Kaunti ya Nyandarua na chuo kikuu cha Nairobi zinatarajia mazuri tume ya elimu ya vyuo vikuu – CUE inapokaribia kutoa uamuzi wa iwapo itaruhusu kufunguliwa kwa taasisi ya elimu ya juu katika kaunti hiyo.
Leo wadau hao waliandaa mkutano wa mwisho wa majadiliano katika taasisi ya mafunzo ya kilimo ya Ol Joroorok ambayo serikali ya kaunti inataka kugeuza kuwa taasisi hiyo itakayohusishwa na chuo kikuu cha Nairobi.
Kaimu naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Margaret Jesang Hutchinson na Gavana Moses Kiarie Badilisha wana imani kwamba CUE itakubalia taasisi hiyo ya elimu ya juu katika kaunti ya Nyandarua.
“Nyandarua ilianza safari ya hamu ya kuwa na taasisi ya elimu ya juu miaka kumi iliyopita na ilikifika kwa Chuo Kikuu cha Nairobi na leo Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu imefanya ukaguzi wa mwisho wa vifaa,” alisema Hutchinson.
Alisema wanatarajia ripoti nzuri ya tathmini kutoka kwa CUE, taasisi ya serikali inayosimamia elimu ya vyuo vikuu nchini Kenya, na hatimaye kutoa idhini kwa ajili ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ya kipekee.
Aliongeza kwamba chuo kikuu cha Nairobi tayari kimetambua wafanyakazi watakaotumwa kwenye taasisi hiyo mara tu idhini ya kuanzishwa itakapotolewa.
Margaret anatumaini kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo kutafaidi wakazi wa Nyandarua pakubwa. Alisema uamuzi wa CUE unatarajiwa kutolewa ndani ya mwezi mmoja.
Gavana Badilisha alisema serikali ya kaunti imekarabati taasisi hiyo ya mafunzo ya kilimo na kuifanya kuwa nzuri tayari kugeuzwa kuwa tawi la chuo kikuu cha Nairobi.
“Tunatarajia KUCCPS (Huduma ya Pamoja ya Usajili wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu vya Kenya) itatupatia wanafunzi kufikia Septemba mwaka huu,” alisema Badilisha.
Gavana huyo alisema kwamba idara za kilimo, elimu na uchumi zitakuwa za kwanza kuanzishwa kwenye taasisi hiyo akiongeza kuwa vitu vyote muhimu kwa elimu ya chuo kikuu kama vile maktaba na intaneti inayoweza kutumika na wanafunzi 300 kwa wakati mmoja vipo tayari.