Msimamizi wa bajeti Margaret Nyakang’o amekatali mbali ombi lililowasilishwa na Seneta Kathuri Murungi, la kutaka kusimamishwa kwa utoaji wa fedha katika hazina ya kaunti ya Meru.
Seneta Murungi, kupitia kwa barua alimtaka msimamizi wa bajeti Margaret Nyakang’o kusimamisha matumizi ya fedha kutoka kwa akaunti ya mapato ya Kaunti ya Meru, akitaja hatua ya bunge la Senate ya kumtimua Gavana Kawira Mwangaza kwa madai ya utumizi mbaya wa mamlaka, ukiukaji sheria na utovu wa nidhamu.
Akijibu barua hiyo, Nyakang’o alisema kufuatia hatua ya mahakama kusimamisha kutimuliwa kwa Gavana Kawira, hana uwezo wa kisheria kusimamiza matumizi ya fedha katika kaunti hiyo.
“Kufuatia agizo la mahakama la kusimamisha kutimuliwa kwa Gavana Mwangaza, inamaanisha kuwa, Gavana huyo yungali afisini hadi mahakama itakapotoa agizo lingine,” alisema Nyakang’o.
Wakati huo huo, wawakilishi wadi wanaomuunga mkono Gavana Mwangaza, wamemshtumu Seneta Murungi kwa kuhujumu maendeleo katika kaunti hiyo.
Pia walilaani maandamano yanayoshuhudiwa katika kaunti hiyo dhidi ya Gavana Mwangaza, wakisema Gavana huyo yuko mamlakani kihalali, kulingana na uamzi wa mahakama.