Huku sherehe za Mashujaa za mwaka huu zikiandaliwa katika kaunti ya Kericho, kaunti hiyo imenufaika na miradi kadhaa ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya kitaifa.
Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni pamoja na kupanuliwa kwa uwanja wa michezo wa Kericho Green, kuweza kukimu watu 10,000, pamoja na ujenzi wa kilomita 10 za barabara.
Hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kericho pia haikuachwa nyuma, kwani ilipandishwa hadhi kutoka level 4 hadi level, hatua itakayosababisha wakazi wa eneo hilo kupata huduma za afya zilizoimarishwa.
Aidha uwanja wa ndege wa Kerenga pia ulifanyiwa ukarabati, na kupanuliwa ili ndege kubwa za kubeba abiria ziweze kutua na kupaa katika uwanja huo. Serikali ilitoa kitita cha shilingi milioni 400 kukamilisha ukarabati wa uwanja huo.
“Uwanja huu wa ndege utapanuliwa na kuwa wa ukubwa sawa na uwanja wa ndege wa Wilson. Uwanja huu utatoa fursa za kibiashara na kufanikisha shughuli za kitalii katika eneo hilo,”alisema Gavana wa Kericho Eric Mutai.
Wakazi wa kaunti hiyo, walipata fursa ya kushuhudia sherehe za aina hiyo karibu nao, huku wanabiashara wakivuna pakubwa kutokana na idadi kubwa ya wageni waliozuru kaunti hiyo kuhudhuria sherehe za Mashujaa.