Wanachama wa Kamati ya bunge la taifa kuhusu elimu wamehoji idara ya Uhamiaji kuhusu kucheleweshwa kwa utoaji wa vitambulisho almaarufu Maisha Card kwa wanafunzi.
Hatua hiyo wanasema imezuia wanafunzi wa vyuo vikuu kupata mikopo na ufadhili wa masomo.
Katika mkutano ulioongozwa na mwenyekiti Julius Melly, katibu wa uhamiaji Julius Bitok alihakikishia wabunge hao kwamba kucheleweshwa kwa utoaji wa vitambulisho vya Maisha Number unashughulikiwa.
Melly alisisitiza umuhimu wa kusuluhisha kucheleweshwa huko hasa kwa vile vyuo vikuu vimeanza kutumia mbinu mbadala, kama vile nambari za NEMIS, kuruhusu wanafunzi kujiandikisha na kuanza masomo.
“Kama Kamati tumeingilia kati kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanaweza kujiandikisha na kupata msaada wa kifedha kwa kutumia NEMIS, wakisubiri vitambulisho lakini tatizo linaendelea. Tunahitaji suluhu,” alisema Melly.
Bitok alikiri ucheleweshaji huo, akitaja changamoto za kiufundi na kisheria ambazo zilizuia utengenezaji wa Kadi za Maisha.
Aliifahamisha Kamati hiyo ya elimu ya bunge kuwa mrundiko wa kadi 600,000 umeongezeka lakini akatoa hakikisho kwamba masuala hayo yametatuliwa.
Mheshimiwa Malulu Injendi, mwanachama wa kamati hiyo, alitaka kufahamishwa kuhusu takwimu kamili za kadi za maisha zilizotolewa na maombi ambayo bado hayajashughulikiwa.
Bitok alijibu akisema Kadi za Maisha milioni 1.8 zimetayarishwa huku zaidi ya milioni 1 zikichukuliwa na wamiliki.
Alisema kadi 569,000 bado hazijachukuliwa na kwamba wameongeza masaa ya kazi kila siku ili kushughulikia maombi yanayozidi kuongezeka.
Dick Maungu alitafuta maelezo kuhusu namna ya kuwasiliana na waliotuma maombi ya maisha Card hasa wanafunzi ili waweze kufuatilia kufahamu iwapo ziko tayari.
Bitok alisema mchakato wa uhakiki wa kaunti za mpakani, ambao awali ulisababisha ucheleweshaji, umefutwa, na kufanya mchakato huo kuwa wa haraka na bila karatasi.
Wasiwasi uliibuliwa na wanachama wa Kamati hiyo kuhusu usalama wa data iliyopachikwa kwenye Kadi za Maisha.
Rebecca Tonkei alihoji usalama wa habari hizo na alijibiwa na Bitok kwamba deta hiyo iko salama.
“Wakenya hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa zao za kibinafsi.” alisisitiza Bitok.
Wanakamati walisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wote wanapokea vitambulisho vyao kabla ya kumaliza masomo ya shule ya sekondari.