Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo leo Jumanne ametathmini athari za mafuriko katika maeneo yaliyoathiriwa katika kaunti mbili za magharibi mwa nchi za Busia na Kisumu.
Lengo la tathmini hiyo lilikuwa kubaini kiwango cha uharibifu, kusimamia usambazaji wa bidhaa za msaada na kushiriki mazungumzo na familia zilizopoteza makazi wakati serikali ikizidisha juhudi za kukabiliana na janga hilo.
Akiwa katika kanti ndogo ya Bunyala, Dkt. Omollo alizuru shule ya msingi ya Lunyofu zinakokaa familia 500 zilizopoteza makazi. Aliongoza shughuli ya usambazaji wa chakula na bidhaa zingine ikiwa ni pamoja na mchele, maharage, mablanketi na vifaa tiba.
Aliahidi kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha usalama wa familia zilizopoteza makazi na kwamba zinarejelea hali ya kawaida.
Akikiri kuwa zaidi ya familia 3,000 katika kaunti ya Busia zimeathiriwa na mafuriko, Katibu huyo amesisitiza umuhimu wa kuzitafutia makazi katika maeneo salama. Pia ametangaza mipango ya kustawisha miundombinu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuzuia maji.
“Ingawa mvua zinatarajiwa kupungua hivi karibuni, lazima tuendelea kuchukua tahadhari na kutii maagizo ya usalama ya serikali. Hii inajumuisha kuepuka maeneo hatari ikiwa ni pamoja na mabwawa, barabara na madaraja yanayochukuliwa kama yasiyokuwa salama na kufuata notisi za uhamaji,” alishauri Dkt. Omollo.
Baadaye, Katibu huyo alienda Kisumu na kutembelea kambi ya waliopoteza makazi ya Ogenya zinakoishi familia 1,973.
Kote nchini, mafuriko yamesababisha familia zaidi ya 3,970 kupoteza makazi , kuvuruga usafiri na shughuli za kilimo na kusababisha vifo vya watu 12. Mtu mmoja bado hajulikani aliko.