Katibu Muthoni: Uwekezaji mwafaka utadumisha wahudumu wa afya Afrika

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu katika Wizara ya Afya nchini Mary Muthoni ametaka uwekezaji mwafaka ufanywe katika miundombinu ya afya, mafunzo, sera na mazingira bora ya utendakazi ili kudumisha wauguzi barani Afrika.

Akizungumza wakati wa kufungua kongamano kuhusu eneo la Afrika lililoandaliwa na baraza la kimataifa la wauguzi mjini Montreal, Canada, katibu huyo alisema kwamba uhamiaji wa wauguzi kutoka Afrika ni changamoto kubwa kwa mfumo wa afya na jamii kwa jumla.

“Ni lazima tushughulikie suala hili kupitia kwa ushirikiano ili kupunguza idadi ya wanaohama, kuboresha mifumo ya afya na hatimaye kuboresha afya ya jamii,” alisema Muthoni.

Muthoni pia aliomba wauguzi watumie fursa zilizopo katika teknolojia ya matibabu kushughulikia dharura na kubadili afya ulimwengini na kusababisha mabadiliko katika afya.

Alisihi wauguzi waungane katika kupigania mabadiliko, kutaka huduma bora za afya kwa wote na kushughulikiwa kwa maswala ya kijamii yanayozingatiwa ili kuunda sera za sekta ya afya.

Alisema wauguzi wanafaa kuharakisha mabadiliko, kupigania haki za walio katika mazingira magumu, kuzungumza kwa niaba ya waliotengwa na kuendeleza sera ya afya kuwa haki ya kimsingi kwa kila binadamu.

Huku akipongeza wauguzi kwa kujitolea kuboresha huduma za afya barani Afrika, Muthoni aliwataka wabadilishane ujuzi na wajifunze kutokana na yale ambayo kila mmoja wao amepitia.

“Naomba kongamano hili liwe chombo cha kuharakisha mabadiliko chanya na chanzo cha ukurasa mpya katika safari ya kuafikia huduma bora za afya kwa wote.”

Website |  + posts
Share This Article