Filamu ya katuni (uhuishaji) ya Kichina “Nezha 2”, ambayo ni muendelezo wa “Nezha 1: Kuzaliwa kwa Mtoto wa Shetani” hivi karibuni imefuatiliwa sana kote duniani. Baada ya kuingia kwenye nafasi ya tano katika mapato ya filamu zilizoonyeshwa kanda ya Kaskazini ya bara la Amerika na ya tatu huko Australia katika wikiendi iliyopita, filamu hii imeipiku “Jurassic World” na kuingia katika nafasi ya tisa katika orodha ya filamu zilizopata mauzo makubwa duniani.
Haya siyo tu ni mafanikio ya filamu hiyo ya Kichina, bali pia ni onyesho lingine lenye mwangaza wa kujiamini kwa utamaduni wa China. Kutoka kuibuka kwa “Nezha 1 ” iliyoonyeshwa mwaka 2019 hadi “Nezha 2” inayopata mafanikio mapya, mfululizo wa filamu hii ya katuni inayosimulia hadithi ya utamaduni wa jadi wa kichina, kupitia kujihusisha na thamani za kisasa na matumizi ya teknolojia ya ngazi ya juu, inaonyesha nguvu kubwa ya utamaduni wa China katika dunia ya leo.
Katika “Nezha 2,” timu ya utengenezaji imefanya marekebisho ya ubunifu kwenye hadithi hii ya kidhahania ya China. Kwa kupitia kuangalia kwa undani hisia ya mhusika na uchambuzi wa kina wa utu, sura ya Nezha imepewa maana mpya inayokubaliana na enzi hii. Uasi wake na ukuaji, au upinzani na uokoaji, vyote vinaweza kupata mwito mkali wa kiroho wa vijana wa zama za leo, bila kujali ni nchi gani anapotoka. Haina shaka kwamba watazamaji wote watakumbuka mstari maarufu kutoka kwenye filamu hii: “Mimi ndiye mtawala wa hatima yangu mwenyewe, sio mungu.”
Marekebisho haya siyo kwamba yanakwenda kinyume na utamaduni wa jadi, bali yanazingatia kwa usahihi maadili ya jumla ya kimataifa huku yakiheshimu msingi wa ukweli wa kitamaduni. Wakati huohuo, michoro ya milima na mito, mitindo ya majengo, mavazi, na mengineyo katika “Nezha 2” pia yamejikita katika uzuri wa utamaduni wa Kichina, lakini pia kupitia teknolojia ya kisasa ya uhuishaji, imeonyeshwa kwa njia mpya sana ya kisanii. Huu ni mtindo wa uonyeshaji unaohifadhi uzuri wa Kimashariki, huku ukizingatia mahitaji ya watazamaji wa kisasa.
Kwa upande wa teknolojia, filamu hiyo imetekeleza maendeleo makubwa katika kiwango cha utengenezaji wa filamu za uhuishaji za Kichina. Kutoka kujieleza kwa uso wa wahusika hadi ujenzi wa mandhari kubwa, na hadi athari za kipekee za picha, kila picha katika filamu hiyo inaonyesha ustadi wa timu ya utengenezaji katika kutumia teknolojia ya hali ya juu. Katika filamu, iwe ni mapigano makali kati ya wahusika wakuu—Nezha na Ao Bing, au mafuriko yanayotokea mwishoni mwa filamu katika mahali alipozaliwa Ne Zha yaani “Chen Tang Guan,” kila picha imejaa nguvu.
Mafanikio ya picha hizi hayategemei tu teknolojia ya kisasa, bali pia yanatokana na uelewa wa kina wa timu ya utengenezaji kuhusu urembo wa kimashariki. Kwa mujibu wa mwongozaji wa filamu, alikiri kwamba awali alitafuta watu wa nchi za nje kutengeneza baadhi ya athari ngumu za picha, lakini hazikufikia matarajio yake. “Mtindo na mbinu za nje labda hazikufaa maudhui yetu na uzuri wetu wa kiutamaduni,” alisema na kwamba “uzuri wa utamaduni wa Kichina lazima uundwe na Wachina wenyewe.”
Hali halisi ni kuwa katika soko la filamu la kimataifa lenye ushindani mkubwa, mafanikio ya “Nezha 2” hayakuja kibahati tu, bali ni matokeo ya kujiamini kwa utamaduni wa China na juhudi za kukuza ustawi wa tamaduni kwa miaka mingi ndani ya nchi. Hasa miongoni mwa vijana wa China wa leo, hisia ya kujivunia kwa utamaduni wao wa asili inaendelea kuimarika. Hii ndio sababu filamu za “Nezha” zimejitokeza kwa njia ya kipekee, tofauti na mitindo ya viwanda ya Hollywood na pia tofauti na mbinu za uhuishaji za kijapani.
Dunia haipaswi kuwa na Hollywood pekee. Inatarajiwa kwamba watazamaji wengi zaidi wa kimataifa wataitazama filamu hii kutoka China, na pia inaaminiwa kwamba kutakuwa na filamu nyingine nyingi zinazoonyesha utamaduni bora wa jadi wa kienyeji kama “Nezha 2” zitakazong’ara kwenye jukwaa la kimataifa, na kuchangia mawasiliano na kufunzana kati ya ustaarabu tofauti wa binadamu na maendeleo anuwai ya tamaduni mbalimbali duniani.