Kinara mwenza wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja Martha Karua amepuuzilia mbali ripoti ya kamati ya maridhiano ya kitaifa iliyotolewa Novemba 25.
Karua kupitia kwenye mtandao wake wa X, amesema ripoti hiyo iliyoundwa na kamati iliyoongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kinara wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah kuwa iliyo na matatizo na haikubaliki.
Karua ambaye ni kiongozi wa chama cha Narc Kenya, ameahidi kutoa taarifa zaidi wiki ijayo kuhusu maoni yake ya kuipinga ripoti hiyo.
Karua alikuwa amesimama kidete akisema kuwa kamwe angeikataa ripoti hiyo kama haingeshughulikia swala la kupanda kwa gharama ya maisha linalowabana Wakenya.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga Jumatano iliyopita aliitaja ripoti hiyo kuwa isiyo kamilifu na yenye dosari lakini inaweza kurekebishwa.
Baadhi ya masuala yaliyoidhinishwa na tume hiyo ni kuundwa upya kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, kuhamisha shughuli zote ugatuzi zizosalia kutoka serikali kuu hadi kaunti, kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani na manaibu wake wawili, kujumuishwa kwenye katiba kubuniwa kwa afisa ya Waziri mwenye Mamlaka Makuu na kuongezwa kwa muda wa kusikiza na kuamuliwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya urais kutoka siku 14 hadi 21.