Katibu anayehusika na huduma za urekebishaji tabia Salome Beacco amefungua karakana ya kisasa katika jela ya wanawake ya Meru.
Karakana hiyo ina vifaa vya kuoka na vile vya kushona nguo, vitakavyotumiwa na wafungwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa karakana hiyo, Beacco alidhihirisha furaha yake huku akishukuru Daktari Manu Chandaria na wakfu wa Chandaria kwa usaidizi wa kifedha uliowezesha ujenzi wa karakana hiyo.
Ilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 12 na katibu alisema ni ya pili baada ya ile iliyojengwa katika jela ya wanawake ya Langata.
Wanawake katika jela hiyo waliwezeshwa pia na vifaa watakavyotumia kuanza kujifunza kuoka na kushona nguo na mtaji wa shilingi milioni 1,203,776.
Kulingana na Beacco katiba ya Kenya inatoa hakikisho la usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na serikali ya Rais William Ruto imejitolea kuhakikisha hayo yanatimia.
Alisema mipango ya mafunzo katika taasisi za kurekebisha tabia itasaidia wafungwa kupata uwezo tena na baadaye kuweza kutoa mchango katika jamii.
Kamishna wa kaunti ya Meru Jacob Ouma alisema kama maafisa wa usalama nchini wanafanya kila juhudi kuhakikisha usalama hauvurugwi kwa njia yoyote.
Jaji wa mahakama ya Meru Edward Muriithi snaye alisema kwamba idara ya mahakama na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma zinatekeleza mpango wa kuangalia upya vifungo kwa nia ya kupunguza msongamano kwenye jela za humu nchini.
Kamishna mkuu wa jela nchini John Warioba alisema mradi uliozinduliwa utatoa mafunzo na pia kukuza matumaini na kujenga msingi wa wafungwa kukubalika katika jamii baada ya vifungo vyao.
Alisema wafungwa wa kike 200 walio katika jela ya Meru watanufaika pakubwa kutokana na mradi huo.