Mwanamuziki wa Marekani Kanye West anaripotiwa kuafikia makubaliano nje ya mahakama na kampuni ya Addidas kuhusu mkataba kati yao uliositishwa ghafla.
Hatua hii inaashiria kukamilika kwa kesi zote zilizokuwa mahakamani na inafuatia miaka miwili ya mivutano mahakamani.
Kampuni ya Addidas iliamua kusitisha mkataba na mwanamuziki huyo baada yake kutoa matamshi yaliyochukuliwa kuwa ya kuunga mkono ubaguzi dhidi ya wayahudi mwaka 2022.
Mkurugenzi mtendaji wa Adidas Bjorn Gulden alisema hakuna kesi iliyo wazi kwa sasa na hakuna pesa zozote watabadilishana na mwimbaji huyo.
“Kulikuwa na mivutano kuhusu masuala mengi lakini pande zote zimekubaliana kwamba hakuna haja ya kuvutana zaidi.” alisema Gulden akiongeza kwamba mambo hayo ni ya kale.
Mwaka jana kampuni ya Adidas ilitangaza kwamba itauza bidhaa zilizosalia za nembo ya Kanye ya Yeezy ambayo ni ushirikiano wake na Addidas na kisha kutoa fedha zitakazopatikana kama mchango.
Wakati huo bidhaa zilizokuwepo zilikuwa za thamani ya zaidi ya dola bilioni moja. Kufikia Julai 2023 Addidas ilipokea maombi ya jumla dola milioni 565 ya viatu vya Yeezy.