Kanye West anaripotiwa kukera majirani zake kwa tangazo lake katika eneo la makazi ya kifahati huko Los Angeles nchini Marekani.
West alichapisha bango katika eneo la Larchmont linaloelezea kwamba anatafuta waimbaji wa kiume ambao ni wamarekani weusi kwa ajili ya kwaya yake iitwayo “hooligan choir”.
Kwaya hiyo inafanyia mazoezi yake kwenye ghala moja lililo karibu na shule moja ya msingi.
Ameelezea kwenye vijikaratasi alivyosambaza kwamba anaotafuta hawawezi kuwa wanono, wawe wamevaa mavazi ya rangi nyeusi na rangi ya ngozi iwe sawia na ya mwanamuziki Sean “Diddy” Combs.
Haya yanajiri wakati ambapo kesi dhidi ya Diddy inakaribia kuanza ambapo analaumiwa kwa ulanguzi wa binadamu kwa matumizi ya kingono.
Masharti mengine ya waimbaji anaotafuta Kanye ni pamoja na mtu kutokuwa na shida ya kuvaa mavazi yenye nembo mbali mbali.
Kando na mabango hayo majirani pia wamelalamika kuhusu kelele inayotoka kwenye ghala ambapo majaribio ya uimbaji yanafanyika.
Wanasema wamefahamisha maafisa wa polisi wa Los Angeles kuhusu usumbufu huo lakini hakuna hatua imechukuliwa hadi sasa.
Nyimbo mbili za Kanye ambazo ni “Carnival” na “Black Skinhead” zinarudiwa mara kwa mara kwa sauti ya juu katika eneo hilo huku watu ambao wamenyoa vipata na kuvaa mavazi ya rangi nyeusi wakionekana kwenye foleni kwa ajili ya majaribio.
Nembo mbali mbali zinasemekana kuchapishwa kwenye ukuta ulio mkabala na shule hiyo ya msingi ikiwemo nembo ya Nazi, hatua ambayo huenda ikaathiri wanafunzi.