Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, amebatilisha agizo lake la hapo awali la kupiga marufuku maandamano Jijini Nairobi, akisema kuwa hajapiga marufuku maandamano hayo.
Mnamo Julai 17, 2024, Kanja alipiga marufuku maandamano Jijini Nairobi, akitaja kuwa habari za kijasusi ziliashiria maandamano hayo yangekumbwa na ghasia.
Kupitia kwa taarifa leo Ijumaa, Kanja alisema maagizo ya Jumatano iliyopita, yalilenga kufahamisha umma kuhusu vitsho vya usalama vilivyohusishwa na maandamano yaliyopangwa kufanyika Alhamisi.
“Ni muhimu kufafanua kwamba, hatujapiga marufuku maandamano ya umma,” alisema Kanja.
Aidha, Kanja aliwakumbusha umma kuwafahamisha maafisa wa polisi kuhusu maandalizi ya maandamano, kuambatana na sheria ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja.
“Tunakumbusha umma kuwa kuambatana na sehemu ya 5(3)(a) na (c), yeyote anayelenga kuandaa mkutano wa hadhara au maandamano anapaswa kumfahamisha afisa anayesimamia kituo cha polisi kupitia maandishi angalau siku tatu na sio zaidi ya siku 14 kabla,” alisema Kanja.
“Ilani hiyo inapaswa kuwa na majina kamili na anwani ya waandalizi, sehemu ya mkutano huo au njia itakayotumiwa wakati wa maandamano,” aliongeza afisa huyo mkuu wa polisi.
Hatua hiyo ya Kanja inajiri siku moja baada ya Mahakama Kuu kusimamisha maagizo hayo ya Kanja, hadi kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute itasikizwa na kuamuliwa.
Jaji wa Bahati Mwamuye akisimamisha agizo hilo, alimzuia Kanja na afisa yeyote wa huduma ya taifa ya polisi dhidi ya kutekeleza agizo hilo.