Huduma ya taifa ya Polisi (NPS), imekanusha kuwa Inspekta Jenerali Mkuu Douglas Kanja, anajihusisha na siasa baada yake kuzungumza katika mojawapo wa mikutano ya Rais William Ruto inayoendelea mlima Kenya.
Wakijibu lalama kutoka kwa chama cha mawakili humu nchini (LSK), huduma ya polisi imemtetea bosi wao, ikisema kuwa uwepo wake katika mikutano ya kisiasa ya Rais Ruto ni mojawapo wa majukumu yake kisheria ya kuhakisha usalama wa kutosha haswa kwa kiongozi wa nchi.
NPS imesema kamwe Kanja, hajajishirikisha na vitendo vinavyohujumu kazi yake na idara ya polisi kwa jumla na kuwataka Wakenya kupuuza taarifa kuwa polisi wanashiriki siasa.
Aidha, NPS imesema kuwa Kanja amekuwa kwenye ziara kadhaa tangu katikati ya mwezi jana katika kaunti za Samburu, Laikipia, Meru, Baringo, Kirinyaga na Nyeri,kukagua oparesheni za kulinda usalama, kukagua vituo vya polisi, kutathmini maslahi ya polisi, kuongoza mazungumzo kuhusu afya ya akili na matumizi ya pesa miongoni mwa maafisa wake.
Idara ya polisi na jeshi zimehutumiwa kwa kujihusisha na siasa tangu wiki jana baada ya Mkuu wa Majeshi Charles Kahariri kuwaonya Wakenya dhidi ya matamshi ya ‘Ruto Must Go’, na pia baada ya Kanja kusimamishwa katika moja wapo wa mikutano ya kisiasa ya Rais na Naibu Rais Kithure Kindiki, na kuwahutubia wananchi kwa lugha yake.
NPS imekariri kuendelea na majukumu yake ya kudumisha usalama kwa wananchi.