Wabunge wamemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, kukabidhi majukumu ya usimamizi wa wafanyakazi, hususan mfumo wa malipo, kwa Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi (NPSC), ili kufanyiwa ukaguzi wa hesabu.
Agizo hilo lilijiri baada ya Kanja hapo awali kuizuia NPSC kuingilia mfumo wa malipo wa Huduma ya Taifa ya Polisi.
Wabunge hao walitoa agizo hilo leo Jumanne, baada ya Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi kulalamika kwamba imenyimwa haki ya kukagua mifumo ya malipo ya Polisi, kufuatia dosari iliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Nancy Gathungu.
Huku akipongeza hatua hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Huduma ya Taifa ya polisi Peter Lelei, alidokeza kuwa Tume hiyo ndio mwajiri halali wa polisi iliyo na mamlaka ya kikatiba kuajiri na kushughulikia maslahi ya maafisa wa polisi.
Aidha alipofika mbele mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Umma, Inspekta huyo wa polisi alisema wamesitisha uhasama uliokuwa kati ya Huduma ya Taifa ya Polisi na Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi.