Kanisa limetakiwa kushirikiana na serikali kuwaelimisha Wakenya kuhusu fursa mbalimbali zinazotokana na mipango ya maendeleo inayotekelezwa na utawala wa Kenya Kwanza.
Mkewe Rais Rachel Ruto ameangazia fursa zinazotokana na mipango ya serikali ikiwemo Hazina ya Ujasiriamali ya Wanawake, Hazina ya Hustler na uwekaji wa huduma zote za serikali mtandaoni miongoni mwa mingine.
Akizungumza wakati wa hafla ya 10 ya maombi inayoandaliwa kila mwaka iliyofanyika katika eneo la Nyeri Golf Club, Mama Rachel alitambua wajibu muhimu unaotekelezwa na kanisa katika ujenzi wa taifa.
Alitoa mfano wa uendeshaji wa shule na hospitali akisema mwingilio wa kanisa katika utekelezaji maendeleo nchini daima umekuwa mnara wa matumaini katika jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi alisisitiza umuhimu wa kulinda siku zijazo za watoto na vijana nchini hasa kutoka kwa minyororo ya dawa za kulevya.
Gavana Mutahi Kahiga na viongozi kutoka Nyeri ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ya maombi.