Kampuni ya magari ya CMC kufunga milango yake Afrika Mashariki

Tom Mathinji
1 Min Read
Kampuni ya CMC kufunga shughuli zake Afrika Mashariki.

Kampuni ya magari ya CMC, imetangaza kuwa itasitisha shughuli zake katika mataifa ya Kenya, Tanzania na Uganda.

Kupitia kwa taarifa ya kampuni hiyo, hatua hiyo ambayo itatekelezwa kwa awamu inaashiria mwisho wa enzi ya kampuni hiyo katika eneo la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, CMC ilidokeza kuwa itahakikisha uamuzi huo unatekelezwa kuambatana na kanuni za makubaliano ya huduma zake katika ukanda huu.

“Hatua hii imeafikiwa baada ya tathmini ya biashara kuambatana na changamoto za kiuchumi, kudorora kwa sarafu na ongezeko la gharama za operesheni,” ilisema taarifa hiyo.

Licha ya juhudi zinazoendelea za urekebishaji na mpango wa mabadiliko uliozinduliwa mwaka 2023, kampuni hiyo imekiri kuwa hali ya sasa ya kibiashara imebainika kuwa ngumu kudumisha njia endelevu za kibiashara.

Kampuni hiyo imewahakikishia wadau wake, hasa wafanyakazi wake, kuwa imejitolea muhanga kuwasaidia kwa kuhakikisha utaratibu mwafaka unafuatwa ambao hautawaathiri , kwa kuzingatia mikataba yote ya makubaliano.

“Kampuni hii imejitolea kuwasaidia wafanyakazi wakati wa kipindi hiki cha mabadiliko,” ilisema CMC.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *