Kampuni ya muziki ya Almagic Uganda Limited imemtetea mwanamuziki Hajat Stecia Mayanja, baada yake kuitwa na chama chake cha National Peasants Party -NPP.
Stecia aliitwa na chama hicho ambapo anahudumu kama mwenyekiti kuelezea ni kwa nini alihusika katika hafla ya chama tawala cha NRM.
Mwanamuziki huyo alichapisha barua iliyoandikwa na mawakili wa kampuni ya Lunar, waliyoandika kwa niaba ya mteja wao ambaye ni kampuni ya Almagic inayoaminika kumsimamia Stecia kama msanii.
Katika barua hiyo iliyoelekezwa kwa katibu mkuu wa chama cha NPP, mawakili hao walielezea kwamba msanii Hajat Stecia Mayanja alikombolewa na mteja ambaye ni NRM kwenda kutumbuiza kwenye hafla yake.
“Tambua kwamba Hajat Stecia Mayanja Farida ana mkataba kama msanii na mteja wetu Almagic na hivyo ni jukumu ake kutumbuiza wakati na mahali ambapo kampuni imeitishwa msanii kutoa huduma za burudani” ilisema barua hiyo.
Mawakili hao waliendelea kwa kumwambia katibu mkuu wa NPP kwamba hana mamlaka ya kukatiza haki ya Stecia kama msanii kutimiza matakwa ya mkataba wake.
“Mteja wetu amesajiliwa kwenye chama chenu kama mtu binafsi na wala sio kama msanii. Unastahili kuelewa hilo” walisema mawakili hao katika barua.
Walipuuza miito ya Stecia kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama cha NPP na wakakitaka chama hicho kibatilishe wito huo na kimwombe msamaha hadharani.
Stecia alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ya NPP jana saa kumi alasiri lakini kutokana na barua hiyo inaonekana hakufanya hivyo.