Kamati yaundwa kuratibu kumbukumbu ya Raila

Shughuli mbalimbali zimeratibiwa kufanyika kati ya Oktoba 10-17, 2026 kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Raila alipofariki Oktoba 15 mwaka jana.

Martin Mwanje
2 Min Read

Familia ya Hayati Raila Odinga imetangaza kubuniwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi itakayoratibu maadhimisho ya kumuenzi Waziri Mkuu huyo wa zamani mwaka mmoja tangu kifo kutokea kwa chake. 

Kamati hiyo itaongozwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Prof. Adams Oloo kwa kushirikiana na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo.

Nayo itawaleta pamoja wawakilishi kutoka upande wa familia, serikali, taasisi za kisiasa, mashirika ya kijamii, sekta binafsi na wanazuoni.

“Lakini sherehe hizi si za kamati, ni za watu. Kutoka Wote hadi Mombasa, Turkana hadi Kajiado, Busia hadi Garissa, Nairobi hadi Meru na kwingineko. Watu wa Baba wote wamekaribishwa,” alitangaza Mjane Ida Odinga wakati akiwahutubia wanahabari, akiwa ameandamana na Prof. Oloo na Seneta wa zamani wa Busia Amos Wako miongoni mwa viongozi wengine.

“Tunafahamu kwamba Wakenya wengi hawakupata fursa ya kumwomboleza jinsi walivyotamani. Hivyo, wiki hii pia ni fursa ya kuja pamoja kushiriki, kuimba, kukumbuka, kuhadithia na kusherehekea maisha yasiyokuwa ya kawaida tulioshi na Baba Raila Amollo Odinga.”

Hayati Raila alifariki Oktoba 15 mwaka jana wakati akipokea matibabu nchini India, na itatimia mwaka mmoja mwezi ujao tangu kutokea kwa kifo chake.

Hatua ya kuunda kamati ya kuratibu kumbukumbu yake inaoenekana kulenga kuzima mirengo iliyoonekana kuchipuka miongoni mwa baadhi ya viongozi waliotaka kuonyesha wako mstari wa mbele kuratibu hafla za kumkumbuka Raila.

Shughuli mbalimbali zimeratibiwa kuelekea kumbukumbu ya kwanza kuwahi kuandaliwa tangu kutokea kwa kifo cha kinara huyo wa zamani wa ODM.

 

 

 

Share This Article