Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni imetembelea kambi ya Kahawa Garrison katika kaunti ya Nairobi ili kukagua utekelezaji unaoendelea wa miradi mbalimbali.
Kamati hiyo ilitembelea Hospitali ya Kikanda ya Nairobi (NRH), vituo vya uhifadhi wa mafuta na ukarabati unaoendelea wa nyumba za makazi za maafisa wa kambi hiyo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Nelson Koech, wanachama wa kamati hiyo walitaarifiwa juu ya miradi hiyo na Kanali Z. I Golo ambaye ni Kamanda wa kambi hiyo, Brigedia Dkt. Mwika ambaye ni Afisa Mkuu wa Matibabu pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Ulinzi.
Kambi ya Kahawa Garrison ilianzishwa Disemba 12, 1964 wakati wa enzi ya ukoloni ya Uingereza.
Kambi hiyo kwa sasa inahudumu kama kituo muhimu cha operesheni za Vikosi vya Ulinzi nchini Kenya, KDF.
Wanachama wa kamati ya ulinzi walisifia huduma mbalimbali zinazotolewa na hospitali ya NRH ikiwa ni pamoja na huduma za afya ya uzazi na meno, ushauri wa jumla na maabara inayofanya kazi kwa saa 24.
Kufikia mwezi huu, hospitali hiyo iliyoanza kuhudumu Aprili 7, 2022, ilikuwa imeahudumia wagonjwa 39,312 wa kutibiwa na kwenda nyumbani na 2,054 wa kulazwa.
Hospitali hiyo huwahudumia maafisa wa KDF, familia zao na wanajeshi wastaafu.
Wanachama pia walizuru miradi mingine ikiwa ni pamoja na uwanja wa gwaride na kituo cha uhifadhi wa mafuta.
Koech alisifia matumizi bora ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuhakikisha utoaji wa fedha kwa wakati unaofaa kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi muhimu.