Kamati ya bunge la Seneti kuhusu kilimo, mifugo na uchumi wa baharini, inaitaka serikali kuwalipa fidia wakulima walionunua mbole feki ili kuwawezesha kupanda upya mimea wakati huu wa msimu wa mvua.
Kulingana na kamati hiyo, wakulima hao huenda wakakosa mimea msimu huu huku ikiwa haijulikani msimu wa mvua utakamilika lini.
Wanachama wa kamati hiyo, waliitaka serikali kuwachukulia hatua kali waliohusika na uuzaji wa mbolea hiyo bandia, na maafisa wa serikali waliofanikisha uovu huo wawajibikie hatua hiyo.
Wabunge hao waliyasema hayo leo Jumatatu, baada ya kukutana na wakulima walioathiriwa na mbolea hiyo bandia kutoka kaunti za Embu na Kirinyaga, walipokuwa wakichunguza sakata hiyo ya uuzai wa mbolea bandia.
Wanachama hao ambao ni pamoja na Maseneta Alexander Mundigi wa Embu, Francis Wafula Wakoli wa Bungoma, Wahome Wamatangi wa Nyeri na mweneyekiti wao ambaye ni Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, walisema uuzaji wa mbolea bandia ni sawa na ugaidi na uhalifu wa kiuchumi na kwamba washukiwa wanapaswa kushtakiwa kwa makosa hayo.
Magunia 2,320 ya mbolea bandia yaliuziwa Halmashauri ya Nafaka na Mazao, NCPB tawi la Embu yaliyokuwa na nenmbo ya KEL Green NPK 10.26.20.
Wakulima waliotumia mbolea hiyo, walisema hawakuridhika na jinsi mimea yao inavyokuwa shambani.