Kamati ya kutekeleza ripoti ya NADCO yabuniwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM  Raila Odinga, wamebuni kamati ya wanachama watano, kuongoza utekelezaji wa ajenda 10 za makubaliano kati ya chama cha UDA na ODM, pamoja na Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano (NADCO) ya mwaka 2023.

Uteuzi wa kamati hiyo unafuatia kutiwa saini kwa Mkataba wa Maelewano Machi 7, 2025, ambapo pande zote mbili zilikubaliana kufanya kazi pamoja kuimarisha ujumuishaji na mshikamano wa kitaifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa Seneta mteule wa zamani wa ODM Dkt. Agnes Zani.

Wanachana watajumuisha aliyekuwa mbunge mteule Fatuma Ibrahim, mtaalam wa sera katika afisi ya kiongozi wa walio wachache Gabriel Oguda, wakili na mtaalam wa uongozi Javas Bigambo na wakili Kevin Kiarie.

“Sekretarieti ya pamoja itakayoongozwa na Makatibu watendaji wa UDA na ODM, pia imebuniwa kupiga jeki operesheni za kamati hiyo,” ilisema taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Ruto na Raila.

Kamati hiyo itashauriana kwa kina na umma, taasisi za serikali, mashirika ya kijamii, yale ya kidini na sekta ya kibinafsi.

Aidha, kamati hiyo itakuwa ikiwasilisha ripoti yake baada ya kila wiki mbili kwa viongozi wa vyama hivyo, na kwa kamati ya pamoja ya wabunge wa Kenya Kwanza na ODM kila baada ya miezi minne.

Website |  + posts
Share This Article