Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, chini ya uenyekiti wa mbunge wa Belgut Nelson Koech imeiomba Tume ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Mambo ya Nje kufanya uangalizi wa kina inapoteua watu wanaopendekezwa kuwa Mabalozi.
Pendekezo hili linajiri baada ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Dkt. Margaret Nyambura Ndung’u kukataa uteuzi wake kama Balozi wa Kenya nchini Ghana akitaja masuala ya kibinafsi na familia.
“Wizara ya Mambo ya Nje na Mkuu wa Utumishi wa Umma wanapaswa kuwa makini na wenye nia thabiti katika kufanya uteuzi. Wakenya wengi wanastahili nafasi hizi na mamlaka husika za uteuzi zinapaswa kufanya uangalizi wao wa kina,” alisema Koech.
Wakati wa zoezi la usaili linaloendelea la walioteuliwa kuwa Mabalozi, kamati hiyo ilibaini kwamba Dkt. Ndung’u alikuwa mtu wa pili kukataa kwenda Ghana kama Balozi baada ya Vincent Kemosi, aliyekuwa mbunge wa Mugirango Magharibi kukataa wadhifa huo mwezi Aprili, 2024.
Katika barua iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati, Nelson Koech, Dkt. Ndung’u alisema, “Ningependa kutoa shukrani zangu kwa mwaliko wa kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, Januari 10, 2025, katika majengo ya Bunge, Nairobi.”
“Kulingana na Sehemu ya 16 ya Sheria ya Uteuzi wa Umma, Sheria ya Idhini ya Bunge 3 ya 2011, ningependa kuwaarifu kuwa sitafika mbele ya kamati hii kusailiwa.”
Dkt. Ndung’u aliongeza, “Hili limesababishwa na masuala ya kibinafsi na ya familia ambayo, baada ya kuyazingatia, hayataniruhusu kuchukua nafasi ya Balozi wa Ghana kama nilivyoteuliwa na Rais William Ruto, Novemba 19, 2024.”
Kamati hiyo ilisaili watu wengine watatu walioteuliwa kuwa mabalozi ambao ni Dkt. Andrew Karanja, Ababu Namwamba na Noor Gabow.