Kamati ya bunge yalalamikia usimamizi mbaya katika Chuo Kikuu cha Nairobi

Tom Mathinji
2 Min Read
Kamati ya bunge kuhusu elimu yafanya ukaguzi katika Chuo kikuu cha Nairobi.

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu imelitaka Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi kuweka wazi nyaraka zinazoongoza shughuli katika taasisi hiyo kufuatia madai ya usimamizi mbaya.

Hayo yalijiri baadaya kamati hiyo kukagua mifumo ya usimamizi na fedha ya chuo hicho pamoja na madai ya uajiri kinyume cha sheria.

Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly,  waliitisha stakabadhi hizo za mwaka wa fedha 2024/25, ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi, idadi ya wafanyakazi wote, bajeti iliyoidhinishwa na matumizi ya fedha katika kipindi cha mwaka 2023/24 na 2024/25, yakiwemo madeni yanayodaiwa chuo hicho yanayojumuisha mishahara.

“Chuo hichi lazima kishughulikie maswala haya haraka iwezekanavyo. Hatuwezi kuwa na taasisi ambayo inatekeleza mifumo potovu ya uongozi na kifedha,” alisema Melly.

Kamati hiyo ilielezea kutoridhishwa kwake na kile ilichokitaja kubuniwa kwa ofisi ya Afisa mkuu wa usimamizi, na kuongezwa kwa muda wa kuhudumu kwa afisa huyo.

Mbali na hayo, kamati hiyo iliibua wasiwasi kuhusu mpangilio wa wafanyakazi na mageuzi katika mpango wa wafanyakazi.

Kwa upande wake, baraza la chuo kikuu hicho liliihakikishia kamati hiyo kuwa litaandaa nyaraka zinazohitajika ambazo zinaongoza usimamizi wa chuo hicho, na kuahidi kuwianisha mfumo wa usimamizi wa taasisi hiyo na sheria.

Prof. Amukowa Anangwe, ambaye ni mwenyekiti wa baraza la chuo hicho kikuu, alihusisha baadhiya changamoto zinazokabili chuo hicho na usimamizi mbovu wa kihistoria na uhaba wa rasilimali.

“Hatumtetei yeyote. Ni wajibu wa serikali na chuo kikuu hiki kushugulikia maswala yaliyoibuliwa kikamilifu,” alisema Prof. Anangwe.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *