Kamati ya bunge la taifa kuhusu maswala ya sheria inayoongozwa na Samuel Chepkong’a ambaye ni mbunge wa Ainabkoi, imeidhinisha kuongezwa kwa ushuru wa barabara.
Wanachama wa kamati hiyo walipitisha ushuru huo baada ya mkutano na maafisa kutoka idara ya barabara wakiongozwa na katibu Joseph Mbugua.
Ilani ya kisheria nambari 9 ya mwaka 2024, iliyoidhinishwa na wabunge, inalenga kuongeza ushuru wa barabara kutoka shilingi 18 kwa lita hadi shilingi 28 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na diseli.
Hata hivyo, kamati hiyo ilielezea wasiwasi iwapo hatua hiyo itasababisha bei ya mafuta kuongezeka.
Ikizingatiwa wakati huu mgumu wa kiuchumi, haitakuwa vyema kuidhinisha sheria itakayosababisha bei ya mafuta kupanda,” alisema Chepkong’a.
Huku akijibu wasiwasi wa kamati hiyo, katibu Mbugu alihakikishia kamati hiyo kwamba, nyongeza hiyo ya ushuru wa mafuta, haitaongeza bei ya mafuta ya Petroli na Diesel.
“Tunawahakikishia wakenya kwamba hakutakuwa na nyongeza ya bei za mafuta. Tumeweka mikakati ya kuongeza ushuru wa barabara bila kuongeza bei za mafuta,” alihakikisha katibu Mbugua.
Aidha alisema kuwa bei za mafuta hudhibitiwa na serikali, huku bei hiyo ikiwekwa kulingana na bei ya bei ya kuagiza bidhaa za mafuta.