Kamati maalum ya bunge la kitaifa inayochunguza madai ya kuondolewa afisini kwa waziri wa kilimo Mithika Linturi, imeanza mchakato huo rasmi leo Jumatano baada ya kuandaa kikao tangulizi cha pamoja na pande mbili husika kwenye kesi hiyo siku ya Jumanne.
Kamati hiyo ya wanachama 11 inayoongozwa na mwakilishi mwanamke wa kaunti ya Marsabit Naomi Waqo, ilibuniwa wiki jana, baada ya bunge la taifa kupitisha hoja ya kumbandua waziri huyo.
Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati hiyo, mdhamini wa hoja ya kumuondoa ofisini waziri huyo ambaye ni mbunge wa Bumula Jack Wamboka akiandamana na wakili wake George Khaminwa, alisema ana ushahidi wa kutosha kumhusisha waziri huyo na sakata ya mbolea ghushi.
Alielezea imani yake kwa kamati hiyo yenye wanachama kutoka mirengo yote miwili ya Kenya Kwanza na Azimio.
Wamboka ambaye aliwasilisha stakabadhi za ushahidi kwa kamati hiyo na pia upande wa waziri alielezea hofu kuhusu usalama wake.
Aidha Linturi pia aliwasilisha majibu ya mashtaka dhidi yake kwa kamati na upande wa mashtaka hivyo kutoa nafasi kuanza rasmi kuskizwa kwa kesi dhidi yake.